Mwaka mmoja kabla ya muhula wake kukamilika, mwenyekiti wa bodi ya vijana, Bruce Odhiambo amejiuzulu.
Kupitia kwa ujumbe wa barua pepe alioutuma kwa vyombo vya habari, Odhiambo alisema kuwa ameamua kujiuzulu ili kuruhusu uchunguzi kufanywa kufuatia madai ya ubadhirifu wa fedha yanayokumba bodi hiyo ya Hazina ya vijana.
‘‘Kumekuwa na usemi mwingi kuhusu kupotea kwa fedha katika bodi ya vijana na itakuwa vyema nipeane nafasi ya uchunguzi kuendelezwa,’’ Odhiambo alisema, kupitia kwa barua hio.
Odhiambo aidha alisema kuwa yupo tayari kuitwa wakati wowote ili kujibu maswali yoyote kuhusu madai hayo ya ufisadi ila alisema kuwa kwa sasa hayupo nchini kwa minajili ya kushugulikia masuala yake ya kibinafsi na atarejea tarehe Aprili 3, 2016.
Odhiambo amehusishwa kwa pakubwa na kupotea kwa sh180 milioni kwenye hazina ya vijana na ambapo sh65 milioni kati ya hizo zilikabidhiwa kwa kampuni moja jijini Nairobi inayofahamika kama Quorandum Limited.
Odhiambo alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya hazina ya vijana baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa bodi hiyo, Gor Semelang'o kuondoka wakati sawa na aliyekuwa waziri wa ugatuzi, Ann Waiguru.
Odhiambo ni mwenyekiti wa nne kwenye bodi hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka wa 2006.