Mwenyekiti wa Maktaba nchini Kenya Samwel Nyangeso amewauliza washikadau katika sekta ya elimu kushirikiana ili kuinua viwango vya elimu katika Kaunti ya Kisii.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea mnamo siku ya Ijumaa katika Shule ya Msingi ya Nyamuya ilioko katika eneo Bunge la Bobasi wakati wa kufungua rasmi maktaba ya shule hiyo, Nyangeso aliwapa changamoto viongozi kuwa kwenye mstitari mbele kuimarisha masomo katika kaunti hiyo.

Mwenyekiti huyo Pia aliiomba Serikali ya Kaunti ya Kisii kujenga maktaba mbili mbili katika kila eneo bunge ili kupunguza msongamano katika maktaba ya Kaunti na kuwasaidia wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali za kaunti.

“Nawaomba walimu, wazazi, maafisa wa elimu na washikadau wengine katika sekta ya elimu kushirikiana ili kuimarisha viwango vya masomo katika Kaunti ya Kisii na kaunti zingine kote nchini,” alisihi Nyangeso.

Kwa upande mwingine, Nyangeso amewasuta viongozi wanaoingiza siasa katika usimamizi wa shule na kusema hiyo inachangia kuzorota kwa masomo miongoni mwa shule.

“Viongozi wetu wanapenda kuingilia usimamizi wa shule ambayo majibu yake kawaida ni kufanya vibaya kwa shule husika. Nawaomba wajitenge na usimamizi wa shule na badala wazisaidie shule hizo kifedha ili kujenga madarasa zaidi na kushughulikia mahitaji mengine ili kuimarisha viwango vya masomo,” alisema meya huyo wa kitambo wa Kisii katika Serikali za Manispa.

Mwenyekiti Nyangeso alitoa mchango wa vitabu vilivyogharimu Sh200,000 kutoka kwa maktaba huku akitoa mchango wa Sh70,000 zake.