Mwenyekiti wa NACADA tawi la Mombasa Sheikh Juma Ngao ameitaka serikali ya kaunti kuifunga mikahawa yote ambayo imewekwa karibu na nyumba za kuabudu.
Ngao amedokeza kuwa mikahawa hiyo imekuwa ikitatiza shughuli za maombi hasa kwa kupiga kelele.
"Mtu anapoenda msikitini, hawezi kumakinika kwa sababu ya kelele kutoka mikahawani. Jambo hili lafaa lishughulikiwe kwa haraka," aliongeza Bw Ngao.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya sherehe ya Makadara eneo la Tononoka Jijini Mombasa, Ngao alisema kuwa mikahawa hiyo imechangia vijana wengi wadogo kuanza kutumia dawa za kulevya.
Aidha, ameitaka serikali ya kaunti kutotoa vibali kwa mikahawa zaidi kufunguliwa jijini Mombasa, akisema kuwa ile iliyoko kwa sasa ni mingi mno kuliko nyumba za ibada.