Mwenyekiti wa chama cha ODM tawi la Nyamira Victor Ogeto ni kiongozi wa hivi punde kuunga mkono hatua ya muungano wa Cord kutaka kuwaadhibu viongozi wa vyama tanzu wasio zingatia sheria za chama.
Akihutubu mjini Nyamira siku ya Jumapili, Ogeto alisema kuwa vyama vya kisiasa vina sheria na masharti yanayostahili kufuatwa, na iwapo kuna mwanachama yeyote atakayedinda kuyafuata sharti achukuliwe hatua kali za kisheria.
“Hatua ambayo chama cha Wiper Democratic Movement inataka kumchukuliwa Gavana Alfred Mutua si jambo geni kwa kuwa vyama vya kisiasa vina sheria na masharti ambayo yanastahili kufuatwa na kila mwanachama, na yeyote atakayekiuka hilo sharti achukuliwe hatua kali na hata kufukuzwa chamani kwa kuwa hiyo ndiyo demokrasia ya chama," alisema Ogeto.
Ogeto aliongeza kusema kuwa hatua ya kuwachukulia hatua wanachama wa vyama vya kisiasa hatua za nidhamu wanapokiuka masharti ya vyama vyao haiathiri kivyovyote uhuru wa wanasiasa kuwasilisha maoni yao.
“Wakati chama chochote cha kisiasa kinapoadhibu wanasiasa, wanachama wanaokiuka sheria za vyama, hilo halimaanishi kuwa vyama hivyo haviungi mkono uhuru wa watu kuwasilisha maoni yao, ila wanalostahili kufanya wanachama hao ni kujadili masuala hayo kwanza chamani kabla ya kuyaweka hadharani,” aliongezea Ogeto.