Huku tamasha za mashindano ya mziki ya shule za msingi ya viwango vya wilaya yakikamilika siku ya Jumatano, mwenyekiti wa mashindano hayo katika wiyala Kisii ya Kati Bwana Nahashon Ooga amesema kuwa yupo tayari kukuza vipaji vya wanafunzi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika shule ya msingi ya Nyambera, Jumatano jioni baada ya mashindano hayo yaliyokuwa yakiendelea kwa siku mbili kufika ukingoni jana, Ooga alionyesha furaha yake na kupongeza wanafunzi na shule zilizoshiriki mashindano hayo, na kutaja hafla hiyo kuwa iliyofana mno na kuahidi kuwa atajitahidi kuona kuwa walioshiriki na kufuzu kuelekea mashindano ya kaunti wanapiga hatua ya kuendeleza vipaji vyao.

“Tutashirikiana na walimu wa shule zote zilizoshiriki ili kuwapa wanafunzi hawa msaada wanaohitaji ili kuendelea zaidi na talanta za kuimba na kughani mashairi,” mwenyekiti huyo alihoji.

Ooga, ambaye pia ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Nyambera, ambayo ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo, alimpongeza msimamizi mkuu wa elimu katika wilaya hiyo kwa kuwawezesha kupata mabasi yaliyowasafirisha wanafunzi kutoka shule mbalimbali kuja kushiriki mashindano hayo.

Hafla hizo za mziki kwa viwango vya kaunti zitafanyika mwezi ujao tarehe 15, katika shule ya msingi ya Kisii.