Mwenyekiti wa muungano wa wafanyibiashara na wachuuzi kwenye kaunti ya Nakuru wa Nakuru Street Traders and Hawkers Association (NASTHA) amesema maisha yake yamo hatarini.
Kupitia kwa ujumbe alioutuma kwa vyombo vya habari Jumatatu, Simon Ole Nasieku amehimiza idara ya usalama kumpa ulinzi akidai kuwa tangu alipoangazia taarifa za kuibuka kwa kundi haramu la Mungiki kwenye kaunti ya Nakuru, watu wasiojulikana wamekuwa wakifika mahala pake pa kazi.
Hata hivyo akizungumza na wanahabari Jumatatu, Ole Nasieku alikariri kuwa amepiga ripoti hiyo kwa kituo cha polisi cha Central mjini Nakuru.
Ole Nasieku alisema vitisho hivyo vinatokana na msimamo wake kwamba kundi haramu la Mungiki limechipuko mjini humo.
Kutokana na hilo, Ole Nasieku alitaka serikali ya kitaifa na kamati ya seneti kuhusu usalama kumchunguza mwanasiasa mmoja mkuu kwenye kaunti ya Nakuru.