Hofu imetandaa katika kijiji cha Ngarariga, eneo bunge la Limuru, baada ya mwili wa mwanaume kupatikana kando ya barabara Jumatatu asubuhi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwili wa marehemu ulitambuliwa na wakazi kuwa John Nganga mwenye umri wa miaka 22.

Nganga alikuwa amechomwa kwa kisu na majeraha kichwani, huku damu nyingi ikiwa kwenye mahali mwili huo ulipatikana.

Wakazi walilamikia kukosekana kwa usalama eneo hilo, wakilia kifo cha mwanaume mchanga mno ambaye alikuwa na maisha marefu mbele yake.

 “Sisi tuna machozi mengi kuona kuwa kijana mwenye nguvu ameuwawa kinyama namna hii. Kwa nini walimuua?” alisema Kahara Kiarie.

Kahara aliongezea kuwa nchi ambayo haina usalama haiwezi kupata maendeleo ya kiuchumi, kwani wakazi huishi kwa uwoga mwingi.

Chifu wa eneo hilo Michael Kangethe alisema kuwa uchunguzi umeanzishwa dhidi ya mauaji hayo, na kuongezea kuwa tayari polisi wammetia nguvuni mshukiwa mmoja.

“Tunasikitika kifo cha mwanaume huyu lakini tuna imani na polisi kuwa waliofanya kitendo hiki watatiwa nguvuni,”  alisema Kangethe.

Mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City mjini Nairobi.

Naibu wa Spika wa Kiambu, ambaye ni Mwakilishi wa Wadi hiyo, Antony Macharia alikemea sana mauaji hayo.

“Tunaomba serikali kuweka doria eneo hili ili kuzuia uhalifu wa aina hii kutokea tena,” alisema Macharia.