Mtoto mwenye umri wa miaka kumi na mmoja kutoka shule ya Bosire Academy ambaye alisombwa na maji ya mvua mnamo siku ya Jumatano akitoka shuleni amepatikana akiwa amefariki.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kulingana na mwalimu wa shule hiyo Wilfred Makori, mwanafunzi huyo wa darasa la sita katika shule ya kibinafsi ya Bosire Academy alitoka na wenzake kuenda nyumbani ilivyo kawaida, lakini mvua ikaanza kunyesha kabla yake kufika nyumbani ambapo alijikinga katika jumba lililoko karibu.

Bwana Makori aliongeza kusema kuwa baadaye walipigiwa simu na mzazi mmoja akiwafahamisha kuwa mtoto amesombwa na maji ya mvua na kuingia mto Nyakumisaro ambapo wakaazi pamoja walimu walianza kumtafuta bila ya mafanikio.

“Tulishtushwa na kisa hicho na hatujawahi kukumbwa na mkasa kama huu, mwanafunzi huyu alikuwa mwerevu na mwenye furaha,” aliskitika mwalimu Makori.

Kisa hicho kimethibitishwa na kamanda mkuu wa polisi katika kaunti ya Kisii Bwa Simon Kiragu, ambaye alisema kuwa mwili wa mwanafunzi huyo umepelekwa katika hifadhi ya wafu ya hospitali ya HEMA mjini Kisii.

Bwana Kiragu aliwaonya wazazi na wanafunzi kujjitahadharisha na kucheza na maji hasa wakati wa mvua nzito inayoendelea kunyesha mjini Kisii.