Wasi wasi umeghubikia kijiji cha Maraigushu mjini Naivasha baada ya wakazi wa eneo hilo kuuupata mwili wa mwanamke mmoja uliokuwa umetupwa kwenye bwawa.
Uso wa mwanamke huyo mwenye umri wa makamo ulikuwa umefungwa kwa kitambaa, wakaazi wakihofia huenda ni dhihirisho ya mauaji ya kikatili.
Mkaazi John Kamau ameongeza kuwa marehemu hajulikani eneo hilo na huenda aliuawa mahala kwingine na kisha kutupwa kwenye bwawa hilo.
OCPD wa Naivasha Titus Munyoki amedhibitisha hayo akisema kuwa mwili huo umechukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya wilaya hiyo.
Alisema polisi watafanya uchunguzi wa kisayansi ili kutambua majina ya mwendazake.
“Huenda msichana huyo aliwajua wale waliotekeleza maovu hayo ndiposa akafungwa kwa kitambaa” Munyoki alisema.