Wasiwasi na hofu imetanda mjini Naivasha baada ya kupatikana kwa mwili wa mwanamke mmoja aliyeuawa huku idadi ya watu waliouawa eneo hilo ikifikia watatu katika kipindi cha wiki moja.
Mwili wa mwanamke huyo ambao alionekana kubakwa kisha kuuawa ulipatikana Jumatano na wakazi ukiwa umetupwa kwenye mtaro mmoja karibu na kijiji cha Kabati.
Mapema wiki jana kulipatikana mwili wa mwanamke mchanga eneo la Ihindu na Jumatatu wiki hii kukapatikana mwili wa mwanamume mmoja eneo la Kinungi kwenye barabara kuu ya Nairobi kuelekea Nakuru.
MCA mteule wa eneo hilo Esther Njeri ambaye alikuwa wa kwanza kufika eneo la mkasa huo alisema: “Huenda mwanamke huyu aliuawa mahala kwingine na kisha mwili wake kutupwa eneo hili."
Afisaa mmoja wa polisi ambaye jina lake limebanwa amedhibitisha tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi umeanzishwa na mwili huo umechukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha.