Mwili wa mwanamke ulipatikana ukiwa umetupwa kando ya barabara katika eneo la Pipeline viungani mwa mji wa Nakuru.
Akidhibitisha kisa hicho siku ya Ijumaa, Kaimu OCPD wa Nakuru Musa Kongoli alisema kuwa mwanamke huyo anayekisiwa kuwa katika ya umri wa miaka 20 hadi 30, hakuwa na kitambulisho wala stakabadhi yoyote ambayo anaweza kutambuliwa nayo.
Kongoli alisema kuwa huenda mwanamke huyo aliuawa kwa kunyongwa mahali kwingine, na kisha mwili wake ukatupwa katika eneo hilo.
“Tulifika katika eneo hilo baada ya kufahamishwa na umma. Tulipiga picha na kisha mwili huo ukapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Kaunti ya Nakuru,” alisema Kongoli.
Kongoli alitoa wito kwa wakazi na wananchi kwa ujumla kuripoti au kuwasiliana na Kituo cha Polisi cha Central, wanapokosa mmoja wa jamaa zao.
Wakazi wa mtaa huo wa Pipeline walitoa wito kwa polisi kuzidisha doria zao za kudumisha hali ya usalama katika eneo hilo.