Mwili wa mwanamume umepatikana pembeni mwa ufuo wa bahari katika eneo la Likoni.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwili wa msichana kupatikana katika eneo hilo.
Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumatatu, mkuu wa polisi katika eneo la Likoni Willy Simba, alisema kuwa mwili wa mwanaume huyo mwenye umri wa kadri, ulitapatikana na watato waliokuwa wakicheza kando kando mwa bahari siku ya Jumapili.
Inaripotiwa kuwa watoto hao ndio waliopiga ripoti kwa maafisa wa polisi.
“Mwili huo utafanyiwa upasuaji kubaini kiini cha kifo cha mwanamume huyo. Ningependa kuhimiza yeyote ambaye jamaa yake alipotea kupiga ripoti kwa polisi ili kutusaidia kuutambua mwili huo,” alisema Simba.
Aidha, afisa huyo wa usalama aliwahimiza wanaoogelea baharini kuwa makini hasa kipindi hiki ambapo mvua kubwa inazidi kunyesha katika sehemu mbalimbali nchini.