Mwili wa mwanamume umepatikana nje ya baa ya Ujamaa eneo ya Likoni, Kaunti ya Mombasa.
Kwa mujibu wa ripoti za polisi, mmiliki wa baa hiyo Martha Adhiambo, alipiga ripoti baada ya kupata mwili wa marehemu nje ya baa yake.
Akithibitisha kisa hicho, afisa mkuu wa polisi eneo la Likoni Willy Simba alisema kuwa bado hawajabaini sababu za kifo hicho, kwa kuwa mwili huo haukupatikana na alama zozote za majeraha.
“Mwili wa mwanamume wa umri wa makamo umepatikana nje ya baa moja eneo la Likoni ingawa bado tunachunguza kiini cha kifo hicho,” alisema Simba, siku ya Ijumaa.
Mwili huo kwa sasa unahifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali kuu ya ukanda wa Pwani, huku uchunguzi ukiendelea dhidi ya mauaji hayo.
Katika siku za hivi karibuni, kumeshudiwa visa kadhaa vya watu kujitoa uhai katika eneo la Likoni.