Hofu na wingu la Kizaa zaa vimewakumba wakaazi wa eneo la Tala Kaunti ya Machakos asubuhi ya kuamkia Jumamosi pale maiti ya mwanamume mmoja mwenye umri wa makamu ikipatikana imetupwa kwenye Shule ya Msingi ya Tala Township na watu wasiojulikana.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwili wa huo ambao ulithibitishwa kuwa wa mwanamume mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi ya kuwabebea watu mizigo kwa mikokoteni katika soko hilo la Tala kwa muda mrefu sasa inashukiwa kuwa huenda alikuwa akitoka sokoni usiku akielekea nyumbani mwake alipokutana na janga hilo ambalo lilimuacha bila sehemu zake za siri.

“Ulikuwa mwendo wa saa saba usiku pale nlikuwa nyumbani na familia yangu tuliposkia mayowe ambayo baada ya muda mchache yalitulia tulijawa na woga na hatungeweza kutoka nje kuenda kutazama kilichokuwa kikiendelea kwani tulihofia usalama wetu pia,” alisema Jane Mwanzia mkaazi wa soko hilo la Tala.

Kizungumkuti  kinachowakumba wakaazi ni kuwa mbona waliomshambulia mtu huyu wamnyang’anye vitu vyote alivyokuwa navyo,  wamvue nguo zote, wamkate sehemu zake za siri na mwishowe kumuua kiunyama.

Ingawaje visa vya wizi wa kimabavu vimekuwa vikishuhudiwa katika eneo hilo, kisa cha aina hii hakijashuhudiwa kwa muda mrefu sasa.

Kwa sasa maiti hiyo imesafirishwa hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha Kangundo huku uchunguzi wa waliomshambulia ukianzishwa.

Wakaazi hao sasa wameitaka Serikali kuwaahakikishia usalama wao huku wakitaka maafisa wengi zaidi wa Polisi kuongezwa katika eneo hilo.