Huku joto la siasa likizidi kushuhudiwa nchini, viongozi wa mrengo wa upinzani wa Cord Kaunti ya Mombasa wameendelea kushinikiza kubanduliwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi alisema kuwa wataendelea kushinikiza IEBC kufanyiwa mageuzi ili uchaguzi mkuu ujao uwe wa huru na haki.

Mwinyi alielezea haja ya Serikali ya Jubilee kuheshimu mrengo wa Cord, na kukubali kufanyia IEBC mabadiliko ili Wakenya wawe na imani nayo.

“Tutaendeleea kushinikiza kuvunjwa kwa IEBC ili tuwe na uchaguzi wa huru na haki. Lazima serikali iheshimu mrengo wa Cord katika kufanya maamuzi,” alisema Mwinyi.

Wakati huo huo, mbunge huyo amewataka viongozi wa kisiasa nchini kujiepusha na siasa za chuki na uchochezi, alizosema kwamba zinatishia kuligawanya taifa.

Kauli hii inajiri baada ya viongozi wanane waliokuwa wakizuliwa korokoroni kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi kufikishwa mahakamani na kuachiliwa kwa dhamana.