Mzee mmoja katika kijiji cha Ndhiwa, Kisumu, amehukumiwa kifungo cha miaka ishirini kwa kumtorosha msichana wa umri wa miaka kumi na minne ili amuoe bila idhini ya wazazi wake.
Babake mtoto huyo Elijah Owuor alieleza mahakama kuwa Shadrack Owago alimchukua mwanawe kutoka nyumbani kwake mnamo tarehe 5, Agosti 2015 na kumsababisha yeye kutoa taarifa kwa mkuu wa polisi katika eneo la Ndhiwa.
Obote aliongeza kuwa baada ya miezi miwili ya kumsaka mtoto huyo, walipatikana katika kijiji jirani cha Luala Kadawa.
Mtoto huyo aliiambia mahakama kuwa Owago aliishi naye katika chumba kimoja ambako alimnajisi kipindi chote.
Akijitetea, mshtakiwa alimwambia hakimu Benard Kipyegon kuwa wazazi wa msichana huyo walimkabidhi mtoto huyo baada ya kulipa shilingi elfu kumi kama awamu ya kwanza ya mahari.
Aidha aliongeza kuwa hakujua umri hasa wa mtoto huyo kwani wazazi wake walimwambia kuwa alikuwa na umri wa miaka ishirini. Alidai kuwa kutolipa awamu ya pili ya mahari kulipelekea kutoelewana na kukamatwa kwake.
Hakimu alipuuza utetezi wake kwani asili ya msichana ilionyesha kuwa ana umri mdogo sana.
Aidha aliamua kuwa Mtuhumiwa anakabiliwa na hatia mbadala ya kufanya vitendo vichafu na mtoto ambavyo ni kinyume na sheria.
Jamaa huyo alipewa kifungo cha miaka ishirini gerezani na siku kumi na nne kukata rufaa.