Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 56 adaiwa kuuwawa kwa kupigwa risasi katika kijiji cha Mbuwani kata ya Bongwe-Gombato huko Ukunda.

Share news tips with us here at Hivisasa

Boko Mohamed Mwakandandi amepigwa risasi nje ya nyumba yake na kuuwawa papo hapo na watu wasiojulikana mwendo wa saa moja usiku wa kuamkia leo.

Akithibitisha kisa hicho afisa mkuu wa polisi eneo la Msambweni Joseph Omijah amesema kwamba watu wawili waliokuwa na bunduki aina ya AK47 wamemshambulia mzee huyo na kumpiga risasi 2 kichwani na mbili kifuani na hatimaye kutoweka kwa kutumia pikipiki.

Omijah amesema kwamba hadi kufikia sasa hawajafahamu lengo la waliohusika na mauaji hayo kwani hakuna chochote walichoiba kutoka kwa mzee huyo.

Amesema kwamba tayari idara ya ujasusi imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho ingawa amesema kwamba huenda mauaji hayo yametekelezwa na vijana waliorejea humu nchini kutoka Somalia baada ya kupokea mafunzo ya kigaidi kutoka kwa kundi la kigaidi la Alshabaab.