Kila anayejua thamani ya mapenzi bila shaka kabla hajaamua kuoa humtafuta mwimbaji huyu stadi wa muziki wa bango ili aweze kutungiwa nyimbo ya harusi.
Mzee Ngala ndiye mwanzilishi wa muziki wa aina ya bango hapa Kenya, na amekuwa kwenye ulingo huo kwa zaidi ya miaka ishirini.
Hata hivyo, baada tu ya kuanza kuvuma, Ngala alianza kupata ushindani mkali baada ya mtoto wake kuchipuka na kuzuka na kipaji ambacho kilimtia wasiwasi wa kukosa soko.
Mwanawe alianza kuimba muziki uo huo na kwa uzuri ulioonekana kumzidi babake, kiasi cha kualikwa mara nyingi na waandalizi wa sherehe za harusi ikilinganishwa na babake.
Baadaye bandi mbalimbali zilianza kuimba bila hata ya kurekodi muziki wa bango, jambo ambalo mzee Ngala amekiri kuwa lilikuwa changamoto kubwa kwake haswa ikizingatiwa kuwa amekula chumvi kiasi cha kutoweza kusakata bandi.
Yote tisa kumi ni kwamba mzee Ngala anakiri kukerwa na vijana hao wanaochipuka kila uchao na kuimba muziki huo bila ya kuzingatia maadili yanayopaswa kupewa nyimbo za bango.
“Vijana wengi ambao wameingilia muziki wa bango sasa wanageuza mtindo na kuanza kutoa video za wasichana walio nusu uchi, jambo ambalo limekuwa likinigadhabisha kila ninapotazama baadhi ya kanda hizo,” alisema Ngala.
Ngala alisema kila tanzu ya sanaa huambatana na maadili yake, ila kwa sasa kumezuka mitindo mipya ambayo anaitaja kama ya kuvuruga muziki wa bango.
Msanii huyo alisema kuwa muziki huo hapo awali ulikuwa ukiheshimika kwani huchezwa na watu wote pasi ya kuzingatia umri, kwa kuwa ulikuwa unakaririwa kulingana na tamaduni za kabila fulani, na hivyo basi ulichukuliwa kama kioo cha jamii.
Aidha, ameziomba bandi zinazocheza muziki huo kutunga mashairi yanayoambatana na tamaduni za kabila wanalotoka waharusi ili kuweza kuzingatia maadili mema katika jamii.