Maafisa wa polisi kutoka kaunti ndogo ya Subukia wamefanikiwa kuwapata mbuzi 22 kati ya 30 walioibwa na wezi wa mifugo Jumapili usiku katika boma ya mzee Julius Gikonyo.
Wizi huo ulitekelezwa usiku wa manane katika kijiji cha Mbogoini ambapo mbali na kutoweka na mifugo hao wezi hao walimua mzee wa boma hilo.
OCPD wa Subukia Alex Ng’ang’a alisema baada ya kupata habari kuhusiana na wizi huo mwendo wa saa sita usiku, maafisa wa polisi walianza harakati za kuwasaka wezi hao.
Kufikia Jumatatu alasiri polisi walikuwa wamefanikiwa kuwapata mbuzi 22.
“Idadi ya wezi hao haijajulikana. Maafisa wa polisi walipofika katika pahala pa mkasa walipata ganda la risasi la bunduki aina ya AK 47 ambayo walitumia kumuua Julius Gikonyo Kabue wa miaka,70, na kisha kutoweka na mbuzi wake,” alisema Ng’ang’a.
Ng’ang’a alisema kuwa bibiye marehemu Teresia Wanjiku wa umri wa miaka, 62, alisema mumewe alisikia sauti za watu zizini mwa mifugo wake, na akatoka nje kuangalia kilichokuwa kinaendelea.
“Wezi hao walimpiga risasi mzee huyo na kufariki papo hapo. Mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Nyahururu,” alisema Ng’ang’a.
Aliongeza mwanamke huyo hakujeruhiwa kwenye wizi huo na inakisiswa kuwa wezi hao walichukulia hali ya kutokuwepo majirani karibu na makazi ya mwathiriwa kwani eneo hilo liko mahali ndani.
Ng’ang’a lisema maafisa wa polisi wanazidi kuwasaka mifugo walio salia.