Wakaazi wa Rwamburi, Ndeiya kwenye mji wa Limuru wanaomboleza kifo cha mzee mmoja mwenye umri wa miaka 92, baada ya kuchomeka katika mkasa wa moto nyumbani kwake.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Majirani walisema kuwa waliona moto mkubwa katika nyumba ya mkongwe huyo usiku wa kuamkia Jumatatu, na juhudi za kumwokoa mzee huyo aliyekuwa akiishi peke yake zliambulia patupu.

Mwakilishi wa kaunti wa eneo hilo la Ndeiya, Nelson Munga aliomba watoto kuchunga wazazi wao na wakongwe vizuri ili kuzuia tukio lingine kama lile.

“Tunasikitika sana kama wakazi wa Ndeiya kuona mmoja wetu ameaga kupitia uchungu mwingi sana na kuwa alikuwa mzee aliyekula chumvi,” alisema Munga.

“Ninaomba watoto kutosahau wazazi wao kwa kuwaangalia vizuri na kuhakikisha hawaishi peke yao wakati wao wanaenda mbali kutafuta mali. Hakikisha mzazi wako haishi peke yake na anapata mahitaji yake ya kila siku,” aliongezea Munga.

Polisi walichukua mwili wa marehemu ambao ulikuwa jivu tu, na kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Uplands huko Nyambari, Lari.

Ni tukio ambalo liliwashangaza wengi ambao walifika pale kujionea mabaki ya moto huo.

“Nilishtuka sana nilipoarifiwa kuwa usiku kulikuwa na moto ambao uliacha mmoja ameaga na ndivyo nikafika hapa kujionea,” alisema Maurice Njenga.