Kwa muda sasa, wafanyibiashara wa mji wa Keroka wamekuwa wakiteseka bila shida zao kutatuliwa.
Hivi majuzi, mmoja wao alijeruhiwa kwa mzozo wa ukusanyaji ushuru uliozuka baina ya wafanyibiashara hao na maafisa wa serikali za kaunti za Nyamira na Kisii.
Mji huu ulikuwa unatumika kama makazi na afisi ya mkuu wa wilaya ya Masaba ambayo ingali katika kaunti ya Nyamira. Mji huu pia ulikuwa na ungali mpakani, jambo ambalo ndilo chanzo kuu cha mzozo, maanake mji huu kama mingine unazidi kukua pande zote mbili za mpaka.
Mzozo kamili ni kuhusu ni eneo lipi linafaa kukusanywa ushuru na maafisa wa kaunti ipi, na jambo hilo la ukusanyaji ushuru na maafisa wa kaunti zote kunawaathiri wakazi wa eneo hili kwa kiwango kikubwa.
Nchini Kenya kuna mifano mingi ya miji ambayo ipo mpakani lakini haijawahi kushuhudia mizozo kama ya Keroka, Garissa ikiwa mfano.
Serikali ya kaunti ya Nyamira, ambayo ni mmiliki mkuu, na ile ya Kisii zimejaribu kupata suluhu bila mafanikio, huku wengi wamewashinikiza magavana John Nyagarama na James Ongwae kukutana ili wajadili swala hili, lakini wao wametilia masikio pampa, ishara kuwa hakuna aliye tayari kumwachia mwenzake sehemu yake.
Serikali kuu inafaa kuziandikia serikali hizi za kaunti za Nyamira na Kisii wateue jopo maalum litakaloongozwa na serikali kuu hili kutafuta suluhu kuhusu mipaka ya mji wa Keroka.