Mbunge wa Njoro Joseph Kiuna pamoja na kamati ya usalama wilayani humo ikiongozwa na naibu kamshna wa jimbo Mohamed Hassan wamefanya kikao na wakazi wa tarafa ya Lare ili kumaliza mzozo uliopo kuhusiana na usimamizi na usambazaji wa maji safi kutoka miradi ya umma.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi wa maeneo ya Naishi Game, Pwani, Nganoini na Muthiga wamekuwa wakishutumu  kamati ya kusimamia mradi wa maji pamoja na kampuni  moja ya mwekezaji wa kibinafsi kwa jina Sopa Lodge kwa mgao duni wa maji.

Wiki jana, mzozo wa rasilimali hiyo mhimu ulisababisha wananchi wenye ghadhabu kuharibu mifereji ya kampuni hiyo, jambo ambalo lilipelekea maafisa wa polisi kuwakamata baadhi yao kwa madai ya uchochezi.

Hassan amesema maafisa wake walifika katika eneo hilo na kuwatuliza wananchi, akisema kikao cha leo kilikusudiwa kujadili hoja ambazo zimetolewa na wananchi.

Naibu kamshna huyo ambaye amewatahadharisha wananchi kujiepusha na kuchukua hatua mikononi amesema ni sharti wananchi watangamane kwa amani, na pia kushirikiana na wawekezaji ambao kando na kufanyabiashara katika maeneo hayo wanawapa nafasi wenyeji nafasi za kazi.

“Sheria kali za zitachukuliwa dhidi ya wananchi wote ambao badala ya kuafikiana kwa amani iwapo kuna mzozo wanajihusisha na fujo na kuvuruga uwepo wa amani,” alisema Hassan.

Kiuna kwa upande wake amependekeza kuteuliwa kwa kamati mpya ya kusimamia maji ambayo wanachama wake watawakilisha kila eneo ili kuleta usawa na kupunguza uhasama miongoni mwa wakazi.

Aidha kiuna amesema amewasiliana na kampuni husika akisema ameanzisha uchimbwaji wa zaidi ya mito sita katika eneo bunge hilo, miradi ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano na vijana wa huduma ya taifa (NYS).