Kumezuka mzozo mpya baina ya wakulima na wafugaji na katika eneo la Mwabonje kaunti ndogo ya Rabai baada ya halaiki ya Ngombe kutoka kwa jamii ya kuhamahama kuvamia zaidi ya mashamba manne ya wenyeji eneo hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akithibitisha tukio hilo naibu chifu eneo la Mwabonje Raphael Kalu alisema ni zaidi ya ngombe ishirini waliopatikana kwenye mashamba mbalimbali yaliyokuwa na mimea mbalimbali ikiwemo mahindi, mkunde, ndizi na mihogo miongoni mwa mimea mingine.

Kwa upande wake chifu huyo anasema kuwa wafugaji hao wamejitetea wakisema kuwa ng’ombe hao walitoroka wakati wa usiku bila fahamu zao na kuwataka wakulima walioathirika kuzungumza na kumaliza kesi hiyo, jambo ambalo wakulima wamelipinga vikali.

Wakulima hao wamesema kuwa imekuwa desturi kwa wafugaji kuwaachilia mifugo wao nyakati za usiku ili kisha baadae kuwatafuta nyakati za asubuhi ila jaribio hilo limetibuka baada ya mkulima mmoja aliyejenga kinyumba kidogo cha kulala shambani kuwaona ng’ombe hao na kisha kuwajulisha wenzake.

Aidha, wakulima hao wamesisitiza kuwa hawatashiriki mazungumzo yoyote na wafugaji hao na kumtaka chifu kuwashurutisha wafugaji kuondoka maeneo hayo na kurudi walikotoka huku wakihoji kwamba tangia walipofika eneo hilo kumekuwa na kesi zinazohusiana na uharibifu wa mimea kutoka kwa wafugaji hao.

Hata hivyo wameitaka serikali kuingilia kati na kuwatafutia sehemu mbadala wafugaji hao kando na maeneo yaliyo na mashamba.

Ng'ombe wakipumzika baada ya kutoka malishoni, wakulima Rabai wameitaka serikali kuwarudisha kwao wafugaji wa kuhamahama.