Mzozo umezuka baina ya wafugaji wa kuhamahama wa jamii ya Somali na wenyeji katika eneo la Maji ya Jumvi huko Mariakani.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Haya yanajiri baada ya wakaazi wa eneo hilo kutaka kuwaondoa wafugaji hao.

Wakazi hao walidai kuwa wafugaji hao huyavamia mashamba yao na kuwalisha mifugo wao bila ya ruhusa kutoka kwa wanaomiliki mashamba hayo.

Julius Chigogo, mwanachama wa mpango wa Nyumba Kumi katika eneo hilo, alisema kuwa wenyeji sasa wanahofia usalama wao kwani jamii hiyo ya Somali inamiliki silaha kama vile visu na panga.

Aidha, alisema kuwa wafugaji hao hudai kuwa wao hupewa ruhusa na maafisa wa serikali kuwalisha mifugo wao kwenye maeneo hayo.

“Hali hiyo imeleta mzozo kwani wafugaji hao waliweza kuhamishwa kutoka sehemu nyengine za Pwani, walikokuwa wakilisha mifugo wao na kuja kuvamia mashamba yetu,” alisema Chigogo.

Kulingana na Judith Kalekya, mkulima wa mboga katika eneo hilo, jamii hiyo ya Somali huwalisha mifugo wao eneo lolote watakapopata nyasi, pasi kuomba ruhusa kutoka kwa wamiliki wa mashamba hayo.

Kalekya alisema kuwa kwa sasa hali ya sintofahamu inawakumba kwani hawajui hatua ambayo jamii hiyo itachukua, ikizingatiwa kuwa wanasema wamepewa idhini kutoka kwa maafisa wa serikali.

Hata hivyo, Mzee Chigogo amesema kuwa watapiga ripoti kwa polisi ili serikali kuingilia kati swala hilo.