Nabii maarufu kutoka Nigeria Johnson Suleman, ametabiri matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kidini katika ukumbi wa KICC, siku ya Jumanne, nabii huyo alisisitiza kuwa rais aliye madarakani kwa sasa ndiye atakayeshinda uchaguzi huo, huku akiongeza kuwa kutakuwa na mabadiliko katika mambo mengi.
Kiongozi huyo wa kanisa la Omega Fire, alimwambia kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuwa anashirikiana na viongozi wasiofaa, huku akitaja hali hiyo kuwa sababu kuu ya Musyoka kusalitiwa.
Alimwambia Kalonzo jinsi amekuwa akisalitiwa katika siku za hapo awali, ingawa alionekana kutojua kuwa Bwana Kalonzo amewahi kuwa na cheo kikuu serikalini. Hapo ndipo waumini waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo walianza kuzungumza kwa sauti ya juu wakimwambia kuwa Kalonzo amewahishikilia wadhifa wa naibu rais.
Haya yanajiri wakati Rais Kenyatta ako katika juhudi za kuwashawishi viongozi wa Ukambani akiwemo Kalonzo Musyoka kujiunga na muungano wa Jubilee.
Inadaiwa kuwa wakaazi wa Ukambani walimpigia kura Raila Odinga na muungano wa Cord kwa ujumla wakitumai kuwa kiongozi huyo wa chama cha ODM atamuunga mkono Bw Kalonzo ifikapo mwaka 2017.
Kwa mujibu wa wafuasi wengi wa ODM, Bw Odinga hakuibuka mshindi katika uchaguzi wa mwaka 2013 hivyo maelewano kati yake na Kalonzo hayawezi kuzingatiwa.
Wafuasi hao walisema kuwa Odinga ndiye kiongozi wa pekee katika muungano wa Cord aliye na uwezo wa kumngatua Rais Uhuru Kenyatta madarakani.
Hii itakuwa mara ya tatu kwa Kalonzo kusalitiwa baada ya kuahidiwa kuungwa mkono kuwa rais lakini akaishia kuwachwa kwa mataa.
Kwa sasa, haijulikani iwapo nabii huyo atafanikiwa kushawishi maamuzi ya kisiasa ya Bw Kalonzo, ikizingatiwa kuwa hatataka kukosa nafasi katika serikali, kwa miaka mitano ijayo.
Uamuzi wowote wa Kalonzo utaathiri siasa za ukambani kutokana na ushawishi mkubwa alionao katika Kaunti ya Machakos, Kitui, Makueni na baadhi ya sehemu katika ukanda wa Pwani.
Kulingana na taarifa kutoka wa vyombo vya habari nchini Nigeria, nabii huyo alikuwa ametabiri kuwa Rais wa zamani wa Nigeria Jonathan Goodluck, atashindwa kwa sababu ya watu ambao alikuwa anafanya kazi nao kwa wakati huo.
Rais huyo alingatuliwa mamlakani na Rais wa sasa Muhammadu Buhari.