Share news tips with us here at Hivisasa

Mamlaka ya kitaifa ya kupambana na mihadarati (Nacada) itatumia kikosi maalum cha maafisa wa GSU kupambana na matumizi ya pombe na dawa za kulevya msimu huu wa likizo za Krismasi.

Akiongea mjini Nakuru Jumanne asubuhi mwenyekiti wa Nacada John Mututho amesema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa sheria za zinafuatwa na watengenezaji,wauuzaji na waumizi wa vileo kote nchini.

Mututho alisema kuwa matumizi ya pombe na dawa za kulevya huongezeka sana msimu wa Krismasi na kuonya kuwa maafisa wa GSU watakuwa tayari kupambana na watakaovunja sheria za vileo malmaarufu 'Sheria za Mututho'.

“Tumekuwa tukitumia sana maafisa wa polisi wa kawaida lakini wengine wamekuwa wakilemaza vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya na ndio maana tumeamua kubadilisha na kuwatumia maafisa wa GSU,” alisema Mututho.

Aliongeza: “Tutashirikiana na wizara ya usalama wa ndani pamoja na serikali za kaunti kuhakikisha kuwa tunakabiliana na utumizi usiofaa wa pombe ili kuepusha maafa wakati wa sikukuu.”

Aidha Mututho alisema kuwa idadi ya maafisa wa GSU watakaotumwa katika kila mji italingana na ukubwa wa mji na idadi ya vilabu katika mji huo.