Mamlaka ya kukabiliana na utumizi wa mihadarati na vileo nchini imetakiwa kujikakamua zaidi kuhakikisha kwamba sheria inayozuilia watoto kuuziwa pombe imetiliwa mkazo, na wahusika kuchukuliwa hatua kali.
Mbunge wa Nakuru Magharibi Samwel Arama alisema siku ya Ijumaa kuwa utekelezaji wa sheria hiyo utasaidia kuhakikisha kwamba watoto wanaepuka maafa yanayotokana na pombe hizo.
Alisema hayo akikosoa wito wa mwenyekiti wa Nacada John Mututho, kufanya marekebisho ya sheria ili kubadilisha umri ambapo mtu anastahili kuruhusiwa kunywa pombe, kutoka 18 hadi 21.
Arama, kwenye mahojiano ya kipekee na mwandishi huyu amesema hatua hiyo haitasaidia vyovyote kwani hata watu walio na umri mpevu hubugia pombe na kuhusika kwenye ajali za barabarani wanapoendesha magari kiholela.
“Suluhisho la Salgaa ni kuweka kwa mbali matuta barabarani, sio kubadilisha umri huo. Pia barabara ya Salgaa ipanuliwe ili magari yanayosimamishwa karibu na barabara yapate pahali pa kusimama,” alisema Arama.