Naibu chifu wa kata ya Bomariba katika kaunti ndogo ya Kisii Kusini Bi Truphosa Orina amewaomba wakaazi wa eneo hilo kujitokeza ili kumaliza utengenezaji, unywaji na uuzaji wa pombe haramu katika eneo hilo.
Akiongea katika eneo la Bogitaa, Bi Truphosa aliwaonya wakaazi wanaotengeneza pombe na kuuza kuwa siku zao ni za kuhesabika na iwapo hawatakoma sheria itafuata mkondo.
Aidha alisema kuwa msako mkali utaanza mwisho wa wiki hii ili kuwakamata wote wanaohusika na utengenezaji wa pombe ili kupunguza wanaojiushisha na unywaji wa pombe haramu ya chang'aa katika eneo hilo.
"Eneo hili la Bomariba liko nyuma sana kimaendeleo, hii ni kwa sababu wakaaji wamejiushisha na pombe haramu kwa muda sasa hadi watoto hawapelekwi shule inavyositahili kupata elimu. Wazazi wengi wamejiingiza katika unywaji wa pombe jambo ambalo limesababisha kuvunjika kwa ndoa nyingi," alisema Orina.
"Iwapo utakamatwa utazabwa faini ya shillingi zaidi ya elfu kumi na tano mahakamani au kutumikia kifungo cha miezi mitatu," alisema Orina.
"Ni ombi langu kwa wakaazi wa eneo hili ni kupiga ripoti kama jirani yako anatengeneza pombe haramu ama umshauri aimwage kabla sheria kumfikia," aliongeza Orina.