Naibu Gavana wa Kaunti ya Nakuru Joseph Ruto amekanusha madai kuwa serikali ya Kaunti ya Nakuru imelitenga na kulibagua eneo la Ingobor.

Share news tips with us here at Hivisasa

Ruto amesema kuwa serikali ya Gavana Kinuthia Mbugua imetekeleza miradi mingi ya kimaendeleo katika eneo hilo lililoko katika Wadi ya Kapkures.

Aidha, aliyataja madai hayo ya kubaguliwa yaliyokuwa yametolewa na baadhi ya wakaazi wa eneo hilo kama yasiyo na msingi wowote.

Akiongea wakati wa mahojiano afisini mwake siku ya Jumanne, Ruto alisema kuwa serikali ya kaunti haiwezi kufurahisha kila mmoja kwa kuwa kila eneo lina mahitaji tofauti na maalum.

“Kuna miradi mingi ambayo imefanywa katika eneo la Ingobor kama vile ya kuchimba visima vya maji, kujenga shule za chekechea, kukarabati barabara na mengine mengi,” alisema Ruto.

Aliongeza, “Hata tukifanya maendeleo, bado kuna watu watakaolalamika kuwa hatujafanya kitu na hiyo ni kawaida, kwa sababu kila mtu ana mahitaji yake muhimu.”

Juma lillilopita, baadhi ya wakaazi wa Ingobor walitishia kuuhama muungano wa Jubilee kwa kile walichokitaja kama kubaguliwa na seriklai ya kaunti ya Nakuru wakati wa kutoa nafasi za uajiri na hata katika kutekeleza miradi ya maendeleo.