Naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amesema shule zote zinastahili ziwe chini ya uongonzi wa walimu walio na maarifa badala ya kusimamiwa na makanisa.
Akiongea siku ya Ijumaa katika shule ya upili ya wavulana ya Riokindo kaunti ya Kisii, Maangi alisema kuwa shule zote zinastahili kusimamiwa na walimu walio na maarifa kuhusu elimu badala ya kusimamiwa na makanisa.
Hii ni baada ya kusemekana kuwa kuna baadhi ya shule ambazo ziko chini ya usimamizi wa makanisa ambapo masuala ya kidini hupewa kipao mbele badala ya kuwapa wanafunzi nafasi ya kuzingatia elimu.
“Shule zinapaswa kusimamiwa na walimu kwani hao ndio walio na maarifa katika sekta ya elimu. Wanafunzi wataendelea kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa elimu isipopewa kipao mbele katika shule zetu. Hatutengi makanisa bali tunasema kua sio makanisa yote yanayojua ni yapi yanastahili kufunzwa shuleni,” alisema Maangi
Aliongezea: “Makanisa yanaweza kuhusishwa katika mambo mengine lakini sio usimamizi wa shule.”
Aidha, maangi alisema pendekezo lake likifuatwa na wanafunzi wapewe fursa ya kusoma, elimu itanawiri zaidi katika eneo la Kisii.
“Tuwape wanafunzi wetu wakati unaofaa kuzingatia masuala ya elimu ili waweze kupita mitihani ya kitaifa,” alisema Maangi.