Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu Gavana wa Kaunti ya Nakuru Joseph Ruto amewahimiza Wakenya kuwaombea Naibu wa Rais William Ruto na mtangazaji Joshua Sang wanaokabiliwa na kesi katika mahakama ya kimataifa ya jinai ICC ili kesi hizo ziweze kutupiliwa mbali.

Akizungumza katika hafla ya maombi ya kwanza ya Kaunti ya Nakuru yaliyofanyika wakati wa kiamsha kinywa siku ya Ijumaa, Ruto alisema Wakenya wanahitaji kufanya maombi badala ya kuingiza siasa katika swala hilo huku pia akiwataka wakenya kuombea hali ya usalama hapa nchini.

“Tuombee kesi za ICC ili Mungu afanye maajabu. Pia, tuombee usalama kwenye Kaunti ya Nakuru na katika taifa hili kwa ujumla. Tulianza huko Kuresoi tukaomba, tumeenda Mt Elgon na tunaendelea kuomba. Tunaona maombi hayo yanazaa matunda kwani tumeanza kuona ni nani aliyeketi na nani kutoa ushahidi wa uongo kwa ICC,” alisema Ruto.

Spika wa bunge la Kaunti ya Nakuru Susan Kihika naye alisema kuwa kwa wakati mwingi viongozi hujitahidi kutekeleza maswala kwa njia iliyo bora lakini kwa wakati mwingine, hilo haliwezekani.

Pia, alielezea furaha yake kuona kuwa Mbunge wa eneo bunge la Nakuru Mashariki David Gikaria, amekubali kufanya kazi kwa pamoja na Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua.

“Sisi kama viongozi kwa wakati mwingi huwa tunajaribu kadri ya uwezo wetu lakini kwa wakati mwingine, huwa ni vigumu kufanya hivyo. Ninafurahi kwamba Gikaria sasa ameamua kufanya kazi kwa pamoja na kaunti ya Nakuru,” alisema Kihika.