Naibu gavana wa kaunti ya Uasin-Gishu Daniel Chemno anataka kubuniwa kwa sheria ambayo itatoa muongozo kuhusu utoaji mahari.
Chemno alisema kubuniwa kwa sheria hiyo kutachangia kupunguza visa vya wizi wa mifugo haswa katika maeneo ya North-Rift.
Aliongeza kuwa visa vya wizi wa mifugo miongoni mwa jamii za kuhamahama kama vile Turkana na Pokot vitaweza kukabiliwa kama vile ilivyokuwa changamoto ya ukeketaji wasichana kabla ya kubuniwa kwa sheria ya kupinga ukeketaji huo al maarufu FGM.
“Changamoto ya ukeketaji wasichana ilikuwa tishio sana kabla ya kubuniwa kwa sheria kuhusu ukeketaji, lakini baada ya kubuniwa kwa sheria hiyo tamaduni hiyo ilianza kurudi chini, hivyo ndivyo inavyohitajika katika changamoto ya wizi wa mifugo,” alisema Chemno.
Mbali na sheria hiyo kukabiliana na wizi wa mifugo Bw Chemno alisema sheria hiyo pia itasaidia vijana wengi ambao wameogopa kuoa kutokana na mahari ya juu kuona kwa haraka.
Akiongea afisini mwake mjini Eldoret Chemno alidai kuwa gharama ya juu ya mahari imefanya vijana wengi kuogopa kuoa huku wanaotoka maeneo kame wakiiba mifugo kutoka kwa jamii jirani ili walipie mahari.
“Inatakikana kuwe na sheria ambapo kutakuwa na muongozo wa kulipa mahari kisheria, na hii sheria inapaswa kuruhusu vijana wetu kulipa mahari hayo polepole kwa mujibu wa uwezo wao hadi pale watakapomaliza wakiwa wako kwenye ndoa," alisema Chemno.
Naibu huyo wa gavana alitilia mkazo umuhimu wa bunge kuharakisha uundaji wa sheria husika.