Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amesema serikali ya kaunti hiyo inaendelea kutengeneza mswada ambao utasaidia kaunti hiyo kuanzisha mradi wa kutumia teknologia ya kisasa katika shughuli zote za kaunti hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa habari siku ya Jumanne katika mji wa Kisii alipoanzisha shughuli ya kukagua ni hatua zipi serikali hiyo imepiga katika sekta ya teknologia tangu iingie mamlakani, naibu gavana huyo alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii inaendelea kutengeneza mswada huo al maarufu County Investment Cooperation.

“Hii ni njia moja wapo ya kusonga mbele kama serikali ya kaunti na tunahitaji kila sekta iwe ikifanya shughuli kupitia teknologia ya kisasa,” alihoji Maangi.

Maangi aliongeza kuwa,  “Hakuna vile kaunti za hapa nchini zitasonga mbele kama hazitumii teknologia ya kisasa maana karibu kila kitu kinawekwa kwa tarakilishi.”

Wakati uo huo, naibu gavana Maangi alisema tayari teknologia ya kisasa imeanza kufanya kazi katika sekta ya afya huku wakiendelea kuangalia ni mbinu zipi watatumia ili kila sekta ifanye shughuli kupitia teknologia ya kisasa.

“Sekta ya kidigitali itasaidia watu wote wa kaunti hii kubaini maneno yote pamoja na miradi ambayo serikali ya Kisii inafanya,” alidokeza Maangi.