Naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amesema madawa ya kulevya ni kama ugonjwa wa malaria ambao umekuwa changamoto kubwa kwa jamii ya Mkisii, na kusema utumiaji wa madawa hayo unastahili kuangaliwa zaidi kama magonjwa mengine.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea na waandishi wa habari hii leo afisini mwake iliyoko mjini Kisii, Maangi alishukuru kampeni ya kupambana na madawa ya kulevya ambayo imefanyika katika ukumbi wa chuo kikuu cha Kisii kwa siku tatu mfululizo, huku chuo hicho kikishirikiana na tume ya kupambana na madawa ya kulevya  nchini  NACADA.

“Kutumia madawa ya kulevya ni ugonjwa kama ugonjwa mwingine mwilini, mtu akizoea huwa vigumu kuacha kutumia madawa,” alihoji Maangi.

“Wengine wanasema kulewa si ugonjwa, lakini kutumia madawa hayo ni ugonjwa kama malaria, ni heri tutumie pesa kuzuia watu kutumia madawa ya kulevya kwa kuendeleza kampeni ya kuelimisha jamii ya Mkisii hatari za madawa ya kulevya badala ya kutumia pesa hospitalini mtu anapoathirika na utumiaji huo wa madawa,” aliongeza Maangi.

Wakati huo huo, aliomba vyombo vya habari kuelimisha wakenya hatari za kutumia madawa ya kulevya kila siku kama njia mojawapo ya kupunguza utumizi wa madawa hayo katika jamii.

“Kampeni hii ambayo imefanyika hapa Kisii isiwe ya mwisho, naomba muendelee kuelimisha jamii hatari za utumiaji wa madawa ya kulevya,” alisisitiza Maangi.