Naibu wa kamanda mkuu wa kaunti ya Kisii Philip Soi amewahidi wazee wa Magenche waliomtembelea siku ya Alhamisi kulalamikia mzozo wa mpaka kati yao na wanakijiji wengine.
Wazee hao ambao walikuwa na kiongozi wao Kenneth Marando walimwomba kamanda wa kaunti Chege Mwangi na naibu wake, Soi kulishughulikia zogo hilo mapema na haraka iwezekanavyo, huku wakisema kuwa vijana wameanza kutumiwa vibaya na viongozi na huenda vita vikaanza baina ya wanavijiji hivyo.
“Nitahakikisha kuwa jambo hilo limeshughulikiwa kwa uhalisia unaofaa, na nawaomba mwongee na vijana wawe watulivu huku tukishughulikia swala hili,” aliahidi naibu Kamanda.
Ikumbukwe kuwa baraza hilo la wazee kutoka eneo bunge la Bomachoge Borabu walikuwa kwenye ofisi ya kutatua mizozo ya mipaka katika idara ya ardhi kaunti ya Kisii mapema mwezi huu, ambapo walikuja kulalamikia swala hilo, huku madai yakizuka kuwa mmoja wa maafisa wa wilaya amekuwa akipendelea upande mmoja kati ya pande hizo zinazozozana.
Ugomvi huo ulizuka kufuatia naibu chifu mmoja wa sabulokesheni ya Bogisankio (Magenche) kusongeza mpaka kuingia kijiji kingine cha Bogiseri (Embakasi), ambapo iliwabidi wazee wa eneo hilo kuchukua hatua ya kumtembelea Kamanda mkuu wa Kaunti ya Kisii Chege Mwangi ili kulitatua zogo hilo.