Licha ya mfungwa mmoja kumshambulia afisaa wa gereza kuu la Kisii, naibu afisaa mkuu msimamizi wa gereza hilo Benjamin Boit amejitolea kuimarisha na kuboresha uhusiano ulioko baina ya wafungwa na waweka usalama wa gereza hilo.
Naibu huyo alisisitiza kuwa bado mna mwelekeo na uhusiano dhabiti miongoni mwa wafungwa na mafisaa wa kituo hicho.
Akithibisha kisa cha wiki jana ambapo afisa wa gereza hilo alishambuliwa na mfungwa kwa kijembe na kukatwa kwenye pua na kuchanwa kwenye kipaji cha uso, Boit alisema kuwa afisa huyo alikuwa katika shughuli ya kawaida kukagua wafungwa ambapo mmoja wa wafungwa alichomoa kifaa chenye makali na kumjeruhi.
Hata hivyo, Boit alifafanua kuwa afisa huyo alishapata matibabu na anaendelea vizuri kiafya, huku akisema kuwa mshukiwa ambaye amewahi kufungwa kwenye gereza hilo hapo awali atachukuliwa hatua ya kisheria kwa kitendo hicho.
“Tumejitolea na kuhakikisha kwamba wafungwa wanachungwa kwa kufuata sheria pia na mafisaa wetu wanatilia maanani usalama wa wote humu ndani,” Boit aliongezea.
Naibu msimamizi huyo aliwataka wanahabari kuwajibika kwa kutoa ripoti halisi kunapotokea shida, ambapo alishangaa zile habari ziliandikwa kuhusiana na kisa hicho zikidai kuwa afisa aliumiza mfungwa.
Aidha aliwashauri wafungwa kutoa malalamiko yao kupitia kwa afisaa wa uhusiano mwema wa gereza hilo ili kupata utatuzi ufaao.