Naibu Rais William Ruto amewaomba wanasiasa kutogawanya wananchi na kusema ni muhimu kwa wanasiasa kuweka uhasama wao wa kisiasa kando na kufanya maendeleo kwa wananchi wa Kenya.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza siku ya Jumapili katika hafla ya kuchangisha fedha za ujenzi wa kanisa moja ya Katholiki katika eneo la Nyasiongo ilioko katika Bunge la Borabu, Kaunti ya Nyamira, Ruto aliwaomba wanasiasa kuweka tofauti zao za kisiasa kando na kufanya maendeleo kwa wananchi.

“Nchi hii ni ya maendeleo na nawaomba wanasiasa wote kufanya maendeleo na kuacha mambo ya fitina ili Kenya iendelee mbele,” alisema Ruto.

Wakati uo huo, Naibu Rais aliwaomba wakaazi wa eneo la Gusii na wananchi wote kwa ujumla kuunga mkono Serikali za kaunti na kusema Serikali za kaunti zikiungwa mkono maendeleo yataafikiwa kikamilifu.

“Nawasihi wananchi kuchunguza jinsi maendeleo yanafanyika katika kaunti zetu ili tujue ni maendeleo gani yamehitimizwa na ni yapi hayajakamilishwa maanake sisi tunahitaji kuona Kenya ikisonga mbele kimaendeleo,” aliongeza Ruto.

Kwa upande mwingine wakaazi wa Kaunti ya Nyamira walifurahishwa na wito wa Naibu Rais Ruto kwa kusema sharti wajumuishwe kwa maendeleo kwa kuchunguza ni yapi yametekelezwa na Serikali za kaunti.

“Nampongeza Naibu Rais kwa kutujali kimaendeleo na kutuhakikishia kwamba sisi kama wananchi sharti tuchunguze yale Serikali za kaunti zimefanya maana tumekuwa kinyume na hapo awali hatuhusishwi kamwe katika maendeleo ya kaunti,” alihoji John Omwanza, mkaazi wa Nyamira.