Naibu wa Rais William Ruto amesema kuwa serikali ya Kenya imejitolea kupigana na ufisadi, huku akisisitiza kuwa mfanyikazi yeyote wa umma au wa kibinafsi ambaye atapatikana katika sakata ya ufisadi atashughulikiwa kisheria bila ubaguzi.
"Tutawafungulia mashtaka wafisadi, funga makampuni iwapo watahusika na uporaji wa mali ya wananchi, sheria ii wazi," alisema Ruto Jumanne kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Ruto ameongeza kuwa ufisadi una uwezo mkubwa wa kulemaza hataua zozote za maenedeleo nchini, na kuongeza kuwa serikali imebuni makundi ya kushughulikia masuala ya ufisadi kama vile tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi ambayo ana imani nayo .
Naibu wa rais vile vile amedokeza kuwa rais Uhuru Kenyatta atakutana na washirika wa kimaendeleo katika kipindi cha wiki mbili zijazo ili kujadiliana kuhusiana na hatua ambazo zimepigwa katika kupiga vita visa vya ufisadi.
Haya yalijiri katika mkutano wa tatu wa ushirika wa kimaendeleo katika ajira ya vijana ambao ulifanyika katika afisi yake katika eneo la Karen jijini Nairobi.
Viongozi wengine ambao walihudhuria mkutano huo ni pamoja na waziri wa Fedha Henry Rotich, magavana Salim Mvurya, Paul Chepkwony, Abdullahi Ahmed pamoja na makundi ya mashirika kijamii.