Mwenyekiti wa bodi ya elimu katika kaunti ya Kisii Henry Onderi amemwomba waziri wa elimu nchini Fred Matiang’i kutotekeleza jambo alilolisema kuwa shule zitakuwa zinanunuliwa vitabu vya kusoma kupitia afisi kuu za wizara ya elimu.
Jambo hilo ni kinyume na jinsi ilivyokuwa hapo awali wakati shule zilikuwa zinapokea pesa kutoka kwa serikali ili kujinunuliwa vitabu hivyo.
Akizungumza na mwandishi huyu, Onderi alisema ikiwa shule zitakuwa zinapokea vitabu badala ya pesa huenda sekta ya elimu ikumbwe na changamoto tofauti tofauti, na kuomba waziri Matiang’i kutotekeleza jambo hilo kwa sasa.
“Naomba waziri wetu wa elimu kutotekeleza jambo la shule kununuliwa vitabu badala ya kutumiwa pesa kujinunulia maana shule ndizo zinajua yanayoendelea kuhusu upungufu wa vitabu,” alisema Onderi.
Ikumbukwe kuwa waziri Matiangi alisema wakati shule zinapokea pesa ili kunua vitabu pesa hizo hazitumiki zote, na kudai visa vya ufisadi hujiingiza.
Aidha, Onderi alipongeza Matiang’i kwa motisha ya kuhakikisha sekta ya elimu imekuwa na mabadiliko makubwa ili kusonga mbele.