Kwa mara nyengine taasisi za serikali zimekinzana pakubwa katika kutoa uamuzi kuhusiana na maandamano ya Cord ya kushinikiza kubanduliwa kwa makamishna wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, kamanda wa polisi Kaunti ya Nairobi alipinga vikali maandamano hayo huku akisema kuwa huenda yakachangia kuvurugwa kwa amani miongoni mwa wakaazi, kauli ambayo imeonekana kuwa kinaya kwa Idara ya Mahakama nchini.

Kwenye uamuzi wake dhidi ya maandamano hayo, Jaji wa Mahakama ya juu nchini Joseph Onguto alisema mrengo wa upinzani nchini una haki ya kuendelea na maandamano.

Aidha, alisema kuwa ni jukumu la maafisa wa polisi kuwalinda wananchi watakaofanya maandamano, huku akiongeza kuwa maandamano hayo yamekuwa ya amani.

Hapo awali, Waziri wa Usalama wa ndani Joseph Nkaissery aliutaka mrengo wa Cord kutoandaa sherehe zao za kuadhimisha siku ya Madaraka katika bustani ya uhuru kwa madai ya uwezekano wa kuzuka vurugu.

Mahakama ilipinga hatua hiyo baadae na kuidhinisha mrengo huo kuendelea na mkutano wao katika bustani hiyo.

Siku ya Jumanne, Nkaiserry alipiga marufuku maandamano hayo ya Cord kote nchini kwa kusema kuwa yanavuruga usalama.

Swali ni je, taasisi za serikali na Idara ya Mahakama huwasiliana zinapofanya uamuzi?

Ikiwa kunayo mawasiliano, mbona uamuzi unakinzana kila mara?