Kenya ni nchi ya kidemokrasia na mojawapo ya matunda ya demokrasia ni kushiriki kwenye uchaguzi.
Iwapo mbunge, seneta, gavana ama rais hajafanya kazi ya kukuridhisha, mbinu rahisi ya kumng’oa mamlakani bila kumwaga damu ama kusababisha uhasama kati ya jamii yako na zingine ni kujisajili kama mpiga kura.
Kwa muda wa takriban miaka mitano sasa, vijana wamelalama kuhusu ukosefu wa ajira, wanawake wamelalamikia kubaguliwa kwa misingi ya kijinsia, huku wanaume pia wakionekana kutokuwa na la kujivunia.
Kuwafokea na kuwarushia mawe viongozi kwenye mikutano ya siasa sio mbinu mwafaka ya kuikomboa Kenya kutoka kwa mikono ya viongozi wachache wasiojali maslahi ya mwananchi wa kawaida.
Wakati umewadai ambapo vijana wanastahili kugutuka na kuwaonyeshe wazee kwamba wao sio viongozi wa kesho bali leo.
Mbinu ya kueleza wanasiasa wakongwe kwamba hawajafaidi nchi hii kama ilivyotarajiwa kabla ya uchaguzi uliopita ni kujitokeza na kujiandikisha kama wapiga kura kwa wingi.
Hata hivyo, kusajiliwa kama wapiga kura hakutoshi. Itawabidi vijana kujitokeza kuwania viti mbalimbali kwenye uchaguzi ujao badala ya kukaa na kutimiwa wanasiasa.
Pwani ni mojawapo wa maeneo yaliyobaki nyuma kimaendeleo na ni jambo la kusikitisha kuona vijana wakikusanyika katika sehemu mbalimbali za mji wa Mombasa wakipiga gumzo ilhali hawajasajiliwa kama wapiga kura.
Nasa kura ili tuinasue Kenya kutoka kwa viongozi wabinafsi.