Mbunge wa Mvita Abdulswammad Nassir ameahidi kuwasilisha ombi bungeni la kupinga kufungwa kwa kampuni mbili za upakuzi na upakiaji jijini Mombasa.
Nassir alisema siku ya Ijumaa, kuwa hatua hii ni ya kusikitisha kuona kuwa wananchi zaidi ya 1200 watakosa ajira kufuatia kufungwa kwa kampuni hizo pasi sababu za kutosha.
Aidha, aliongeza kuwa atahakikisha kuwa bunge linawachukulia hatua za kisheria wakuu wa halmshauri hizo kwa matumizi mabaya ya afisi.
Nassir ameitaja hatua hiyo kuwa na msukumo wa kisisa kutoka mrengo wa Jubilee, ikizingatiwa kampuni hizo zinamilikiwa na familia za gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye yuko thabiti kuunga mkono mrengo wa Cord.
Alielekeza vidole vya lawama kwa Halmashauri ya KPA na KRA kwa kutumiwa kisiasa.
Kwa sasa zaidi ya watu elfu moja mia mbili wanaofanya kazi katika kampuni hizo hawajajua hatma yao baada ya tukio hilo.
Kampuni hizo mbili za Autoport na Portside Freight Terminals zilifungwa kufuatia barua kutoka kwa Halmashauri ya KRA kwa usimamizi wa kampuni hizo bila kueleza sababu za kimsingi za kufungwa kwake.
Abdulswammad alikuwa ameandamana na mbunge wa Jomvu Badi Twalib, Omar Mwinyi wa Changamwe, Rashid Bedzimba wa Kisauni, mwakilishi wa wanawake Mishi Mboko na mbunge maalum wa Zulekha Hassan miongoni mwa wawakilishi wa bunge la kaunti yab Mombasa.