Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amesema ataongoza maandamano iwapo taasisi za usalama hazitosita kushika wakaazi wa Mombasa bila hatia na kisha kuwaachilia baada ya kupewa hongo.

Nassir aliyasema haya siku ya Jumamosi katika uwanja wa Tononoka akieleza kwamba polisi wamekuwa wakifanya kazi yao ya kutafuta wahalifu lakini wengi wanaokamatwa ni watu wasiokuwa na hatia yoyote.

Aidha, alisisitiza kuwa atahakikisha askari wanaowaangaisha raia wanakabiliwa kisheria ili kulinda haki na uhuru wa mwananchi.

Wakati huo huo, gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho amelipigia upato suala hilo na amevitaka vyombo vya usalama kutowatumia vijana kama vitenga uchumi vyao kwa kuwashika bila hatia na kisha kuwaachilia baada ya kuhongwa.

Kauli hii ilijiri baada ya kushuhudiwa kwa visa vingi vya raia kulalamikia unyanyasaji kutoka kwa polisi katika eneo bunge la Mvita.