Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amesema kuwa maandamano ya kushinikiza kubanduliwa kwa Tume huru ya mipaka na uchaguzi IEBC, yataendelea mjini Mombasa hadi makamshina wa tume hiyo watakapo ng'atuka mamlakani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Nassir alisema kuwa Wakenya hawana imani tena na Tume ya IEBC na lazima tume hiyo kuvunjwa ili kupeana nafasi kwa makamishna wengine kuteuliwa.

Mbunge huyo alisema kuwa huenda uchaguzi mkuu ujao ukakumbwa na kasoro na machafuko iwapo swala hilo litakosa kutatuliwa kwa wakati mwafaka.

Nassir amewahimiza Wakenya kuunga mkono mrengo wa Cord kushinikiza kuvunjwa kwa tume hiyo.

"Sisi tuko tayari kuhakikisha kuwa swala la IEBC linatatuliwa kwa wakati mwafaka na iwapo serikali ya Jubilee inajali maslahi ya Wakenya, basi watuite tujadiliane,” alisema Nassir.

Mrengo huo wa Cord umekiri kuendelea na maandamano hayo hadi pale serikali ya Jubilee itakapokubali kuvunjwa kwa tume hiyo ya IEBC.