Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amesema kuwa ana imani kuwa Muungano Mpya wa Wabunge wa Pwani utaleta mabadiliko katika eneo hilo.

Nassir amesema kuwa muungano huo utakuwa na fursa nzuri ya kuangazia maswala muhimu yanayohusu wakaazi wa Pwani kwa jumla.

Katika tarifa kwa vyombo vya habari baada ya uchaguzi huo siku ya Jumatano, mbunge huyo alisema kuwa changamoto kubwa inayowakumba wakaazi wa Pwani ni usalama na ardhi miongoni mwa changamoto zingine.

“Tuweke siasa kando na tufanye kazi. Huu muungano mpya utaangazia mambo yanayowahusu Wapwani kwa jumla na nina imani kuwa tutachukua hatua kubwa,” alisema Nassir.

Uchaguzi huo ulifanyika katika majengo ya bunge siku ya Jumatano, huku wabunge 19 kati ya jumla ya wabunge 33 kutoka maeneo ya Pwani wakihudhuria hafla hiyo.

Katika uchaguzi huo mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga alichaguliwa kama mwenyekiti huku mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Lamu Shakila Abdalla akichukua nafasi ya naibu mwenyekiti.

Mbunge wa Voi Jones Mlolwa alichaguliwa kama katibu wa muungano huo naye mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa Mishi Mboko akiwa naibu katibu.