Zaidi ya familia 200 kutoka kambi moja ya wakimbizi wa ndani kwa ndani huko Gilgil zililazimika kulala nje kwenye kibaridi kikali usiku wa kuamkia Jumatano, baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko.
Wahanga hao kutoka kambi ya Kingdom Seekers iliyoko karibu na ardhi ya Mbegu wameachwa wakikadiria hasara kubwa kufuatia mvua hiyo ambayo ilinyesha siku mbili mfululizo.
Mwenyekiti wa wahanga kwenye kambi hiyo Naomi Chege amesema kuwa hakuna kilichoweza kuokolewa kufuatia mkasa huo.
“Hatukuokoa chochote, watoto pamoja na wakongwe ndio wameathiriwa pakubwa,” Chege aliambia mwandishi huyu.
“Ni swala ambalo linatutatiza na sijui tutasumbuka hivi mpaka lini. Serikali iskie kilio chetu,” aliongeza Chege.
Huku hayo yakijiri, wakazi wa eneo la Eburru mjini humo wameendelea kukadiria hasara kubwa baada ya barabara inayounganisha kijiji hicho, mji wa Gilgil na Naivasha kukatika kutokana na mvua hiyo kubwa ambayo inaendelea kunyesha.
Walioathiriwa ni wafanyibiashara waliokuwa wakielekea katika soko la Naivasha.
“Juhudi zetu za kutafuta usaidizi kutoka kwa afisi ya mbunge wa Gilgil Mathenge Ndiritu zimekuwa zikigonga mwamba,” Lydia Nyota, mkaazi, alisema.
Juhudi za mwandishi huyu kuzungumza na mbunge wa Gilgil Mathenge Nderitu kuhusiana na hali ya barabara kwenye eneo hilo hazikufaulu baada yake kukosa kujibu simu.