Maafisa wa afya katika jimbo la Nakuru wakishirikiana na bodi ya maziwa wameanzisha msako kuwatia mbaroni wachuuzi bandia wa maziwa.
Maafisa hao wamesema wanalenga wale wanaouza bidhaa ambazo hazijakaguliwa hasa maziwa na nyama na hivyo kuhatarisha maisha ya wale wanaotumia bidhaa hizo.
Afisa mkuu wa afya katika jimbo la Nakuru Samwel King’ori amewataka wakaazi kujiepusha na ununuzi wa maziwa kutoka kwa wachuuzi ambao hawana leseni.
"Bidhaa hizi ambazo zinachuuzwa hazijakaguliwa ipasavyo ni hii ndio sababu wakati mwingine unaona kuna visa vya watu kupata sumu kutoka kwa vyakula wanavyonunua ovyo," alisema King'ori.
“Tumeungana na Bodi hiyo kuhakikisha wakaazi wanapata bidhaa ambazo ni salama kwa matumizi,” aliongeza King’ori.
Wakati huo huo wagonjwa katika hospitali za umma jimbo la Nakuru wanakabiliwa na wakati mgumu baada ya wauguzi kuanza kususia kazi tangu siku ya Jumatano.
Uchunguzi ulioendeshwa na mwandishi huyu katika hospitali ya Kaunti unaonyesha kuwa wagonjwa hawapati huduma kwenye hospitali hiyo.
Madaktari wanaosusia kazi wanashinikiza kupandishwa ngazi kazini na kulipwa marupurupu yao.