Tume ya kitafa ya uiano na utangamano nchini NCIC imetajwa kama tume isiyokuwa na nguvu ama uwezo wa kutekeleza majukumu yake kikamilifu kama inavyohitajika.
Kulingana na afisa wa Haki na sheria katika shirika la Haki Afrika Francis Auma, licha ya viongozi wa kisiasa kuchacha kurushiana matusi na kauli za uchochezi hadharani tume hiyo bado haijawachukulia hatua yoyote.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa katika kongamano la wanaharakati wa maswala ya kijamii, Auma alieitaka tume hiyo kuwajibikia majukumu yake kiukamilifu nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ujao ili kupunguza hofu ya kuzuka kwa ghasia nchini.
"Tunakosa kuielewa hii tume ya NCIC jinsi inavyofanya kazi zake kwa sababu watu wengi hasa viongozi wetu wanaenda kinyume na sheria, na hakuna hatua zozote za kinidhamu wanachukuliwa iwapo wameshindwa na kazi, basi wajiondoe na makamishna wengine wateuliwe," alisema Auma.
Wakati huo huo, Auma ametoa wito kwa wakenya wasikubali kugawanywa na mirengo ya kisiasa au vyama kwani amelitaja jambo hilo kama linalochangia mgawanyiko miongoni mwa wakenya.