Kamishna wa NCIC Adan Mohammed akiwahutubia wanahabari hapo awali. [Picha/ citizentv.co.ke]
Tume ya Uiano na Utangamano wa kitaifa NCIC imetilia shaka hatua ya viongozi wa Pwani kutaka kujitenga.Tume hiyo imesema kuwa hatua hiyo itatatiza amani nchini.Akizungumza siku ya Jumatano kwenye kongamano la washikadau mjini Kilifi, kamishna wa NCIC Adan Mohammed alisema kuwa huenda hatua hiyo ikasabibisha vurugu zitakazo waathiri raia wasiokuwa na hatia.“Huenda hatua hii ikazua vita na kusababisha umwagikaji wa damu nchini, jambo ambalo litahujumu na kupoteza maisha ya wengi,” alisema Mohammed.Mohammed alisema kuwa masaibu ya wapwani yanaweza kutatuliwa pasi eneo hilo kujitenga.“Sio lazima Pwani kujitenga kwani masaibu yanayowakumba wakaazi wa Pwani yanaweza kutatuliwa kwa kufuata sheria pasi kuzua fujo,” alisema Mohammed.Kamishna huyo ameyataja maswala ya ardhi na dhuluma za kihistoria kama sababu kuu ambazo wapwani wanadai kutengwa, na kusema kuwa serikali inajitahidi kusuhulisha maswala hayo.“Serikali inajaribu kila mbinu kutatua swala la ardhi na dhulma za kihistoria ili kila raia apate haki yake ya kikatiba,” alisema Mohammed.Kauli hii inajiri baada ya viongozi wa kisiasa wa mrengo wa NASA eneo la Pwani wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi kusisitiza kuwa watafanya kila mbinu mpaka eneo la Pwani lijitenge kutoka kwa taifa la Kenya.