Wakati ambapo papa mtakatifu ameitaka jamii ya Kenya kutangamana, wito kama huo umetolewa na mwakilishi wa wadi ya Bahati katika kaunti ya Nakuru kusaidia wasiojiweza na walemavu katika jamii.
Peter Nderitu Mwangi amesema ili kuinuana mmoja na mwingine, upendo kwa wasiojiweza ni nguzo muhimu katika kuendeleza Kenya.
Akiongea leo Alhamisi katika eneo la Wanyororo Bahati kwenye hafla moja ya kuchangisha fedha kumsaidia Jane Wambui kurekodi nyimbo zake, Nderitu maarufu kama Birishiba, alisema kwamba walemavu hujihisi kama wasio na maana wakati ambapo wanatengwa na jamii.
“Sisi zote tuliumbwa kusaidiana, ndio maana kuna dereva na abiria, kuna mpishi na mteja, kuna muuzaji duka na mteja. Tunahitaji tu kushirikiana, kuonyesha upendo haswa kwa walemavu na maskini katika jamii. Na huo ndio ujumbe ambao pia Papa Francis ametutolea leo.”
Wambui anaishi na ulemavu wa kutoona, japo ana kipawa cha kutunga na kuimba nyimbo.
Na wakati uo huo Nderitu alihakikishia wakaazi wa eneo hilo kwamba taa za usalama zitawekwa mwanzoni mwa mwaka ujao.
Alisema “Fedha za kuweka ‘mulika mwizi’ eneo la Ahero, Kanduma, Wanyororo, Bahati na Karunga zimo kwenye bajeti ya mwaka huu wa kifedha, naomba uvumilivu wenu”